Kwa mujibu wa kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Muhammad Abdul-Salam, Mkuu wa Ujumbe wa Kitaifa wa Mazungumzo wa Yemen, ameeleza: “Sana’a inawakaribisha wananchi wote wa taifa hili, na milango yake iko wazi kwao wote ili warejee na kushirikiana pamoja na raia wema.”
Abdul-Salam, katika ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake kwenye mitandao ya kijamii, amesisitiza kwamba msamaha uliotolewa na Rais Mahdi Al-Mashat unaonesha kujali kwa uongozi katika kulinda maisha ya watu na kukomesha migogoro ya ndani.
Amewashauri wale ambao bado wako katika safu za maadui wa taifa na wanaochochea vita vya wenyewe kwa wenyewe kurejea katika njia iliyonyooka na katika ardhi ya nchi yao, hususan baada ya kubainika kwamba mradi wa maadui wa taifa ni mradi wa mauaji, migogoro na uvamizi, na kwamba lengo lake ni kuwachosha na kuwateketeza wananchi kwa ajili ya kuhudumia maslahi yao.
Abdul-Salam ameashiria kwamba; kuendelea kuwasajili wanajeshi na kuhamasisha vikosi kwa kushirikiana na pande za kigeni zenye uhasama hakutazaa matokeo yoyote isipokuwa uharibifu na kuongezeka migogoro ya ndani, na kutachangia kuendelea mzingiro dhalimu dhidi ya wananchi wa Yemen pamoja na kuwanyima rasilimali, utajiri, uhuru na mamlaka yao ya kitaifa.
Mkuu wa Ujumbe wa Kitaifa wa Mazungumzo amewashukuru watu wote waadilifu na waaminifu walioondoka katika kambi zinazohusishwa na Saudi Arabia na kurejea kwenye familia zao. Aidha, amesifu kiwango cha juu cha uelewa kuhusu ukweli wa njama za kigeni dhidi ya taifa na juhudi zao za kuidhoofisha na kuigawa nchi kupitia kuchochea vita, matumizi ya silaha na kila aina ya nyenzo za mauaji na uharibifu.
Maoni yako